Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amemuagiza Waziri na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusitisha mara moja utekelezaji wa zoezi la
kuwaondoa wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la Machinga katika
Jiji la Mwanza mpaka hapo mamlaka husika itakapokamilisha maandalizi ya
maeneo watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha wamachinga wenyewe.
Rais Magufuli akiwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa
agizo hilo leo tarehe 06 Desemba, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam huku
akionya kuwa kiongozi yeyote ambaye hayupo tayari kutekeleza agizo hilo
aachie ngazi.
“Kumeibuka tabia ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi
kuwafukuza Wamachinga bila utaratibu wowote wa wapi wanawapeleka na
wakati mwingine wanapelekwa maeneo ya mbali ambayo hayafai hata kwa
kufanya biashara, hili jambo sio sawa hata kidogo.
“Sipendi Wamachinga wafanye biashara kwenye hifadhi ya barabara lakini
hakuna sheria katika nchi hii inayosema mtu wa biashara ndogondogo au
Mmachinga hatakiwi kukaa katikati ya mji, tukianza kwenda kwenye
utaratibu wa namna hiyo maana yake tunaanza kutengeneza madaraja ya
Watanzania, kwamba kuna Watanzania fulani wa daraja fulani wanapaswa
kukaa katikati ya mji na Watanzania wa daraja fulani hawatakiwi kukaa
katikati ya mji, huo sio mwelekeo wetu na wala Ilani ya Uchaguzi ya
Chama Cha Mapinduzi ambayo mimi na wewe (Makamu wa Rais) tulipita
kuinadi, haisemi tutengeneze madaraja ya watu wanaostahili kukaa mjini
na wengine hawastahili kukaa mjini, sasa nimeona hili nilizungumze na
nataka kulirudia kwa mara ya mwisho” amesema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli ameelekeza kuwa Wamachinga waliondolewa katika maeneo yao
Jijini Mwanza waachwe waendelee na shughuli zao mpaka hapo Halmashauri
ya Jiji la Mwanza itakapokamilisha maandalizi ya mahali
watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha Wamachinga wenyewe.
“Narudia na hii ni mara ya mwisho, kawaambieni hata Wamachinga wa Mwanza
warudi kwenye maeneo yao mpaka watakapowatengenezea utaratibu mzuri,
Kigamboni hapa palikuwa na wamachinga eneo fulani wamehama vizuri kweli,
wakatengenezewa miundo mbinu yao katika soko lao na sasa hivi wanafanya
kazi vizuri, na waliwashirikisha viongozi wa Wamachinga, lakini Mwanza
imekuwa ni amri tu na wengine wanatumia hata msemo wa Hapa Kazi Tu, mimi
sikusema msemo wa Hapa Kazi Tu wa namna hiyo, nadhani mmenielewa”
amesisitiza Rais Magufuli alipokuwa akiwaekeleza Naibu Waziri wa
TAMISEMI Mhe. Suleiman Jafo na Katibu Mkuu TAMISEMI Mhandisi Mussa
Iyombe.
Wakati huo huo, Rais Magufuli ameagiza Wizara ya Nishati na Madini
kusitisha mara moja zoezi la kuwaondoa wachimbaji wadogo katika Kijiji
cha Nyaligongo kilichopo katika Kata ya Mwakitolyo Mkoani Shinyanga na
badala yake wachimbaji hao waachwe waendelee na shughuli zao, na leseni
ya mwekezaji anayedai eneo hilo ni lake aondolewe.
“Wale waliofukuzwa Shinyanga wabaki palepale, kama ni leseni ya huyo
mwekezaji ifutwe, Mhe. Makamu wa Rais fuatilia hili, mweleze Waziri wa
Nishati na Madini, waache kufukuza wananchi hovyohovyo, wale wanapata
riziki yao, wanasomesha watoto wao lakini wanafukuzwa tu.
“Na hizi ndio ajira zenyewe, tulisema tunatengeneza ajira, wewe
mwekezaji ni mmoja unakwenda kuwafukuza watu 5,000? haiwezekani na wala
haingii akilini” amesisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli amekemea vitendo vya wawekezaji wakubwa kupewa maeneo
ambayo wachimbaji wadogo wanaendesha shughuli zao tena kwa mtindo kwa
kutengeneza nyaraka zinaonesha mwekezaji husika alipewa eneo hilo kabla
ya wachimbaji wadogo na kusisitiza kuwa mchezo huo hautavumiliwa.
Hata hivyo Rais Magufuli amesema maagizo yake hayana maana kuwa
Wamachinga na Wachimbaji wadogo waendeshe shughuli zao kwa kuvunja
sheria bali wazingatie sheria na Mamlaka zisiwanyanyase watu wanyonge.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
Wednesday, December 7, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment