WAZUNGU wanasema kwa Kiingereza chao, Deal done. Yaani biashara
imekwishamalizika. Watu wananyanyuka katika viti vyao, wanapeana mikono,
wanakumbatiana, wanaondoka. Uhamisho wa Paul Pogba inasemekana
umemalizika.
Manchester United imefanikiwa kumnasa kiungo huyo mahiri wa Juventus kwa
dau la Pauni 100 milioni ambalo litaweka rekodi mpya ya uhamisho
duniani na kulipiku dau la Pauni 85 milioni ambalo Real Madrid walilipa
mwaka 2013 kumchukua Gareth Bale kutoka Tottenham.
Licha ya kulipa dau hilo, United watamlipa Pogba mshahara wa pauni
210,000 kwa wiki kwa mkataba wa miaka mitano ikiwa ni miaka minne tangu
alipomruhusu kuondoka bure kwenda Juventus Julai 2012 akiwa mchezaji
kinda.
Bosi wa Man United, Ed Woodward alikacha kwenda katika ziara ya United
nchini China na alikutana na Wakurugenzi wa Juventus, Giuseppe Marotta
na Fabio Paratici, pamoja na wakala wa Pogba, Mino Raiola kwa ajili ya
kumaliza dili hilo.
Juventus iling’ang’ania dau hilo licha ya Man United kujaribu kushusha,
lakini mwishowe Man United imekubali kulipa dau hilo kwa staa huyo
mwenye umri wa miaka 23 ambaye amezaliwa nchini Ufaransa na wazazi wake
waliotokea Guinea barani Afrika.
Kocha wa Man United, Jose Mourinho alikuwa anamtaka staa huyo kabla ya
pambano la ngao la hisani kati yao na Leicester City Agosti 7 na
atajiunga nao mara baada ya timu hiyo kurejea katika ziara ya maandalizi
ya msimu mpya nchini China ambako wametua juzi.
Pogba aliondoka Old Trafford katika utawala wa kocha mkongwe, Sir Alex
Ferguson baada kushindwa kuhakikishiwa nafasi katika kikosi cha kwanza
kilichokuwa kimesheheni mastaa wakongwe kama Paul Scholes ambaye
Ferguson hakutaka kumuweka benchi na alimuamini zaidi.
Tangu hapo, Pogba ameibuka kuwa mmoja kati ya viungo bora barani Ulaya
huku akiiwezesha Juventus kutwaa ubingwa wa Serie A mara nne,
akiifikisha pia katika fainali za Ulaya pamoja na kuipeleka Ufaransa
katika fainali za Euro 2016 ambapo walichapwa 1-0 na Ureno.
Mfaransa huyo atakuwa mchezaji wa nne kusajiliwa na Man United dhini ya
Mourinho baada ya kuwanasa Eric Bailly kutoka Villarreal, Zlatan
Ibrahimovic aliyenaswa bure kutoka PSG na Henrikh Mhkitaryan
aliyechukuliwa kutoka Borussia Dortmund.
Wakati dau la Pogba likianza kulalamikiwa na wadau wengi wa soka kwamba
haliendani na kiwango chake, tayari nyota huyo ameanza kupata watetezi
akiwemo staa wa zamani wa Arsenal na timu ya taifa ya Ufaransa, Thierry
Henry.
“Sahau kuhusu Ufaransa, nadhani anaweza kuwa mmoja kati ya viungo bora
katika historia. Ana ubora wa kufanya hivyo. Anahitaji kuwa makini tu na
kitu anachoweza kukifanya vizuri.” Alisema Henry katika michuano ya
Euro.
Saturday, July 23, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment