Monday, September 12, 2016

Huo ndio ukweli wenyewe. Tafakari juu ya taarifa ya Benki Kuu inayoonyeha kwamba tangu Magufuli kuingia madarakani kasi ya kukua kwa uchumi wa Taifa imepungua kwa asilimia 4.

Tukiwa na ukuzi wa asilimia karibu 9 kwa mwaka, Tanzania ilikuwa moja ya nchi kinara duniani kwa kukua uchumi. Sasa suala la kujiuliza ni kwamba, kubanwa kwa ufisadi kunakofanywa na Rais Magufuli, ni kubaya kwa kuwa kunasababisha kasi ya uchumi wetu kupungua?

Ukweli ni kwamba ufisadi unaongeza mzunguko wa fedha nchi, kwa kuwa mafisadi hutumia fedha kwa wingi na hivyo kuwa kichocheo cha shughuli za kiuchumi. Matokeo yake wafanya biashara ndogo na kubwa wote wanafaidika na fedha za ufisadi, na kufaidika huku kunaleta kukuka kwa kiwango cha maisha (standard of living) kwa wengi, maana watu wanakuwa wamejaa mapesa. Fedha za ufisadi pia huingia kaitka uwekezaji na hata kutengeneza ajira katika sekta za ujenzi, usafiri, kilimo, nk.

Kimsingi, ufisadi ni sawa na serikali kutoa fedha kwa "taasisi" (stimulus packages) ili kuinua kuchochea shughuli za kiuchimi, kama tu Obama alivyotoa fedha kwa taasisi za Marekani pale hali ao ya uchumi ilipokuwa mbaya sana wakielekea hali ya recession.

Labda kibaya ni kwamba ufisadi unaleta mporomoko wa thamani ya fedha unaotokana na fedha nyingi kuwa mikononi mwa wananchi (inflation). Lakini hili lilipingwa sana na Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia, Zenawi, pale ambapo serikali yake ilitoa pesa kwa wananchi ili waanzishe miradi kama ya mahoteli ya kitalii na majengo ya ofisi, na uchumi wa Ethiopia ukawa unakua kwa kasi sana huku inflation rate ikipanda hadi asilimia 17. Zenawi alisema kwamba hakuona tatizo uchumi wa nchi kukua sambamba na inflation rate.

Sasa, kuzuia ufisadi ni kubaya? Jibu ni hapana, ila sasa, ukiwa Raisi ukabana sana ufisadi kiasi cha kupunguza mzunguko wa fedha nchini, inabidi uangalie mianya ya kuongeza mzunguko wa fedha, mbadala wa ufisaidi. Kwa mfano, kosa linalofanywa na serikali ni kubana ufisadi na bado kuweka kodi nyingi ambazo zinabana watu kufanya biashara. Angalia jinsi bandari ilivyokauka, hatua iliyochukuliwa sambamba na kubana ufisadi. Ufisadi wa kuingiza bidhaa kwa kukwepa kodi mara nyingi ni matokeo ya kuwapo mfumo unaoumiza wa utozaji ushuru na kodi kwa bidhaa toka nje ya nchi.

Kwa hiyo basi, Raisi Magufuli anapaswa kuangalia upya suala zima la utozaji kodi nchini, kwa kuwa amebana ufisaidi. Kodi zinatakiwa zilegezwe mno, katika principle ya "economies of scale". Kwa mfano, ule mfumo wa kukadiria na kutoza kodi kabla hata biashara haijaota miguu inapaswa ubadilishwe. Pia kodi na hata ushuru wa bidhaa toka nje zinatakiwa zishushwe ili kuwapa hata wale wenye mtaji mdogo nafasi ya kuagza bidhaa za kiuwekezaji. Biashara ndogo ndogo ambazo hazizidi mtaji wa kama milioni kumi zinaweza kusamehewa kodi kabisa. Na pia kuwe na mfumo tofauti wa kodi kulingana na wapi muwekezaji anawekeza; kama ni jiji, mkoa, wilaya au kijijini. Unaweza hata kusema ukijenga kiwanda kijijini basi kodi yako inapata punguzio la asilimia 50, tofauti na kama ukikijenga kwenye jiji.

Kwa hiyo serikali ya Raisi Magufuli inapaswa kuchukua haraka hatua za kurekebisha mfumo wa kodi hasa kwa kuwa mianya ya ufisadi imezibwa. Kumbuka kwamba ufisadi ni sawa na kumbebesha mtu ndoo ya maji inayovuja. Kuvuja kwake ni nafuu ya mchukuzi, lakini ukiziba kuvuja bila kumpa ahueni ya kupumzika kwa namna fulani, utakuwa unamwumiza badala ya kumsaidia.

0 comments:

Post a Comment