Ni kweli inauma mno kutelekezwa na mzazi. Mimi ambaye baba na mama yangu
walinilea kwa umoja wao pamoja na umaskini wetu, huwa nawaza ingekuwaje
baba au mama asingekuwa karibu yangu? Malezi ya mzazi mmoja au wote
wasingekuwepo. Inaumiza sana!
Hiyo ndiyo sababu naweza kuhisi kile ambacho kinamuumiza mtoto
aliyetelekezwa. Mimi ni baba, najua ni kiasi gani mtoto wangu
ananihitaji kwa ukaribu. Upendo wangu kwake umekuwa zawadi yake muhimu
kutoka kwangu kuliko kitu chochote. Hivyo basi, najua atapitia machungu
kiasi gani kama nikimtelekeza.
Chukua hii; Kwa hali yoyote ile, mzazi hana leseni ya kumtelekeza mtoto
wake. Changamoto zije na ziondoke, hakikisha unabaki umemganda mwanao.
Kosa la kumtelekeza mtoto linafanana na la kuua. Huyo ni mtoto wako,
unamkimbia, unataka alelewe na nani?
Mwanamuziki Aboubakar Shaban Katwila ‘Q Chilla’ katika nyimbo zake Aseme
na Si Ulinizaa, alionesha wazi kuumizwa na alivyokataliwa na baba yake,
Shaban Katwila, tangu akiwa mimba.
Baba mcheza soka maarufu Tanzania, mtoto anaishi kwa shida, akisaidiwa
na wasamaria wema, wakati huo mama mzazi alishafariki dunia. Q Chilla
akaokotwa! Ukitafakari vizuri unaweza kuhisi Q Chilla aliumia kiasi
gani.
Baada ya vilio vingi, mzee Katwila alitumia njia mbalimbali kutengeneza
suluhu na mwanaye. Wakasameheana na kudumisha upendo kama mtu na mzazi
wake. Tangu hapo, Q Chilla alipitia vipindi vingi vibaya, baba yake
akawa msaada wake.
Mara ya mwisho nilipozungumza na Q Chilla, alikiri kuwa yupo kwenye
kipindi kizuri sana cha maelewano na baba yake na kwamba alikuwa mmoja
wa watu waliompigania aweze kuacha matumizi ya dawa za kulevya baada ya
kutopea.
Chukua hii; Watu hufanya makosa lakini ni haohao hugeuka watu wazuri.
Anaweza kukutenda leo lakini kesho akakufaa. Ni mwongozo wa wahenga kuwa
hupaswi kutupa jongoo na mti wake.
Isisahaulike migogoro ya kimapenzi husababisha maumivu mengi kwa watoto,
vilevile uchonganishi kati ya mtoto na mzazi mmoja. Mama akibaki na
mtoto baada ya kutofautiana na baba yake, anaweza kumjaza mtoto sumu
kuwa baba yake alimsusa, hakumjali.
Hutokea kwa akina baba ambao hulea watoto bila mama zao, nao hutema sumu
yenye uchonganishi kati ya mtoto na mama yake. Ni vizuri sana mtoto
anapopevuka ayapime matukio ya nyuma kwa kutumia akili ya kikubwa.
Anaweza kupata majibu ambayo ni mazuri mno kwa maisha yake.
Kwanza mzazi ambaye anamtelekeza mtoto wake ni mtu ambaye anastahili mno
kuhurumiwa, maana hawezi kuwa sawasawa. Binadam aliyekamiliki kiakili
anatambua kuwa mtoto ni sehemu ya maisha yake, hatathubutu kumtelekeza.
Stadi wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul Juma ‘Diamond Platnumz’ ana machungu
yake. Alishapata kueleza kuwa baba yake, Abdul Juma hakuwa na muda naye
kipindi anakua, hivyo jukumu la malezi na ukuaji wake, lilisimamiwa na
mama yake, Sanura Kassim ‘Sandra Khan’.
Malezi ya Diamond yalijaa machozi na jasho, mama yake akihangaika huku
na huko kuhakikisha mtoto wake anapata mahitaji muhimu, japokuwa
haikuwezekana kupata yote. Kwamba wakati huo wa mateso, baba yake
aliendekeza utoto wa mjini, akashindwa kuzingatia kuwa yeye ni baba.
Diamond naye ameamua kutoa adhabu kali kwa baba yake. Hamshirikishi
kwenye mafanikio yake. Wengi tu wanakula matunda ya kazi yake ya muziki
ambayo imempa umaarufu mkubwa barani Afrika na kwingineko duniani, baba
mtu haambulii chochote.
Baba Diamond anapigika, anaumwa anakosa mpaka msaada wa matibabu, wakati
huo Diamond anatapanya fedha kwa watu wengine. Inawezekana anafanya
hivyo kutokana na hasira kali alizonazo, ila zimezidi kipimo.
Leo hii Diamond hana ubavu wa kumfuta baba yake kwenye mzunguko wa
maisha yake, isipokuwa atabaki kuwa baba yake anayemchukia. Na je, hizo
chuki hazifiki mahali zikaisha?
Kuna adhabu kubwa ambayo Diamond anashindwa kuitumia, na yenyewe ni kuwa
chanya kwa baba yake. Angekuwa anamjali na kumpa huduma nyingi muhimu,
angekuwa anamsuta kwa vitendo, kwamba yeye alimtelekeza kisha
anamhudumia.
Uamuzi wa Diamond kutomjali baba yake ni kisasi. Na ni mwendelezo wa
damu mbaya ambayo mara nyingi huhama kutoka kwa mzazi mmoja kwenda kwa
mwingine.
Leo hii Diamond ni baba, yupo vizuri na mwanaye kwa sababu hakuna
mgogoro kati yake na mama wa mtoto wake ambaye pia anatarajia kumzalia
mtoto wa pili. Mama ni raia wa Uganda, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss
Lady’, mtoto aliyepo ni wa kike, Latiffah, wanatarajia wa kiume.
Inaweza kutokea baadaye Diamond akagombana na Zari kisha akawa mbali na
watoto wake kwa sababu ni wadogo. Mama akatumia nafasi yake kuwajaza
sumu watoto wake kuwa baba yao aliwatelekeza. Nao wakikua wakamchukia
baba yao. Diamond anatakiwa ayapime hayo.
Huu ni wakati mzuri mno kwa Diamond kukata mnyororo wa chuki kati yake
na baba yake. Kutosikia kilio cha baba yake ambaye anaumwa ugonjwa
mkubwa (kansa), ni roho ngumu mno. Ni roho ngumu mithili ya ile ya
Jenerali Idd Amin Dada wa Uganda.
Diamond anayo nafasi ya kumhudumia baba yake kama ambavyo mtu anaweza
kujitolea kwa ajili ya raia wengine wenye matatizo wanaomgusa.
Kiusamaria wema tu. Ajitolee tu!
Namkumbusha kuwa alimnunulia gari aliyekuwa mkongwe wa muziki nchini,
marehemu Marehemu Muhidin Maalim Gurumo, baba yake akiwa anaishi
katikati ya dhiki kubwa. Vilevile amekuwa akinukuliwa kutoa misaada
mbalimbali, baba yake anateseka. Misaada sharti ianze nyumbani.
Hiyo chuki mpaka lini Diamond? Mbona hujakana kutumia jina lake? Unaitwa
Nasibu Abdul Juma, huyo Abdul Juma unamwacha anataabika kwa sababu ya
visirani vya nyakati za giza. Tafadhali Diamond usiwe na roho ya Idd
Amin, haikufai. Zipo baraka nyingi utaongezewa baada ya suluhu yako na
baba yako.
Wednesday, September 14, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment