Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemtaka Gavana wa Benki Kuu (BoT)
Benno Ndulu, na Mwendeshaji wa benki ya FBME, Lawrence Mafuru, wafike
mahakamani kujieleza jinsi watakavyotekeleza amri iliyoitaka BoT kulipa
Sh bilioni 92.
Maofisa hao wanatakiwa kuieleza mahakama
watakavyoilipa kampuni ya Coast Textiles Ltd fedha hizo na kama
watashindwa kufanya hivyo, watafungwa jela kama wafungwa wa kesi ya
madai.
Utekelezaji wa amri hiyo unatokana na uamuzi wa shauri
namba 129 la mwaka 2009, ulioiamuru benki ya FBME kuilipa kampuni ya
Coast Textiles Ltd fedha hizo baada ya kukamata kiwanda chake na kukiuza
kwa kampuni ya Five Star Investment ltd.
Uuzwaji wa kiwanda hicho ulitokana na mgogoro wa ulipaji mkopo ambao kampuni ya Coast iliuchukua katika benki hiyo.
BoT
inahusishwa kwenye shauri hilo kutokana na kuchukua uendeshaji wa benki
ya FBME baada ya benki hiyo kuhusishwa na utakatishaji fedha nchini
Cyprus.
Maofisa hao walitakiwa kufika mahakamani hapo Septemba 16
mwaka huu kwa ajili ya kueleza jinsi watakavyotekeleza amri hiyo,
lakini hawakufika kwa kuwa wamewasilisha maombi ya kusimamisha shauri
hilo ambayo yamepangwa kusikilizwa leo mbele ya Jaji Ama Munisi.
Katika
kesi ya msingi iliyofunguliwa na kampuni ya Coast, mahakama iliamuru
FBME iilipe kampuni hiyo Sh bilioni 21.2 na riba ya asilimia 21 kwa
mwaka tangu Juni 28, 2001 hadi hukumu ilipotolewa, Julai 27, 2015.
Baada
ya uamuzi huo, walalamikaji walipeleka maombi ya utekelezwaji wa hukumu
hiyo, ambayo ukijumlisha na riba ni sawa na Sh bilioni 92.2.
Kutokana
na maombi hayo, mahakama ilimuelekeza Gavana wa BoT kukamata akaunti
mbili zinazomilikiwa na benki ya FBME, hata hivyo BoT iliwasilisha
maombi ya kuchunguzwa kwa umiliki halali wa akaunti zinazoshikiliwa na
kuiomba mahakama isitishe amri hiyo kwa kuwa BoT siyo miongoni mwa
walalamikiwa kwenye shauri la msingi.
BoT iliingilia kati suala
hilo, kwa kuwa kwa sasa ndiyo inayosimamia uendeshwaji wa benki ya FBME
kwa ajili ya kulinda amana za wateja baada ya benki hiyo kuhusishwa na
utakatishaji fedha.
Baada ya kusikiliza maombi hayo, mahakama
iliondoa amri hiyo na kuamuru benki hiyo ilipe fedha, hata hivyo
walalamikaji waliwasilisha maombi mengine ya kukazia hukumu katika
Mahakama Kuu.
Katika maombi hayo Msajili wa Mahakama Kuu, Projest
Kahyoza alitoa siku saba kwa maofisa hao kufika mahakamani kujieleza
jinsi watakavyolipa fedha hizo na wakishindwa watafungwa jela kama
wafungwa wa madai.
Thursday, September 22, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment