Muziki wetu una changamoto nyingi sana zinazoikabili. Mara nyingi
tumekuwa tukiangazia yanayofanyika katika muziki wenyewe ambayo ni
rahisi kuonekana, mfano aina ya muziki kwa kuigiliziana/mkumbo, au njia
wanazotumia wasanii wetu katika Kufikisha kazi zao.
Lakini mimi leo nimeona niangalie upande mwingine kidogo ambao ni fursa
kwa wasanii na vijana wengi ambao wanaangalia muziki kama wasanii tu,
waandaji, na waongozaji video kama ndio sehemu pekee za kuweza kuingia.
Muziki ni tasnia/sekta kama sekta zingine ambazo hazijajitosheleza ili
kujisimamia moja kwa moja kama wenzetu walioendelea, bado pesa zinavuja
mahala ambapo kunahitaji usimamizi, bado mambo hayaendi kwa uweledi au
kwa mfumo unaotambulika na kuweza kuwafanya vijana (wasanii, waandaaji,
waongozaji) wawe matajiri na kuweza kusaidia makundi mengine na
kuongeza pato kwa taifa, ili tujivunie vipaji na uwepo wao.
Hapa naangalia sehemu ya uongozi ambayo inahitajika kuwaongoza wasanii
wetu na kuwafanya wawe bidhaa bora ambazo zitaweza kuwasogeza kutoka
hapa walipo na kupiga hatua zinazotakiwa mbele, wasanii wamekua
wakiipigia kelele serikali irasimishe sanaa lakini bado wanasuasua, sasa
inabidi wasanii waamke na kuamua kujinyanyua wenyewe mpaka hapo
serikali itakapo amka na kuwaunga mkono, maana ni lazima watakuja tu
wakiona mmesogea.
Fursa ipo kwenye umeneja, ni wakati sasa wasomi wetu ambao wana shahada
mbalimbali kama masoko, uhasibu, au hata utawala wenye hamasa na sanaa
wakatizamia upande huu wa muziki ambao una uhaba wa mameneja katika
kuwaongoza wasanii wetu waweze kua na mipango iliyoandaliwa kitaalamu na
mikakati mizuri kuanzia kujitengeneza kama bidhaa na muziki kwa
ujumla.
Inaweza kuwa labda nawaza kitu ambacho kinahitaji sijui utaalamu wa
kisanaa lakini nachoona wasanii wetu wanahitaji kwa ukubwa ni watu wa
kuwasimamia ili wawalipe sio mameneja ndio wawalipie vitu vyote wasanii
wetu. Tunahitaji watu ambao watalipwa na wasanii, watakua chini ya
wasanii.
Au ni wakati sasa wasanii wetu waanze kuangalia umuhimu wa kupata
uongozi ambao utaweza kuwasimamia kila kitu kuweza kufikia malengo yao,
uongozi ambao utaweza kuwatafutia matamasha ya kutumbuiza, masoko ya
kuuza miziki yao, mpaka makampuni ya kuweza kuingia nayo ubia au
kutangaza bidhaa zao au kua mabalozi, pamoja na kuwaongoza katika mstari
ulio nyooka.
Maswali huwa najiuliza: Ni wasanii wetu wamekosa uweledi wa kuona
umuhimu wa kuwa na watu watakao wasimamia kwa kuwachagua wao? Au ni
kumekosekana watu mahiri wa kuweza kuonekana na wasanii ili wapewe hio
kazi? Au ni watu wenyewe hawajafunguka na kuona kama kuna fursa ya
kwenye muziki?
Au niseme umefika muda wa kutotafuta nani mchawi na kuanza kwa kila
mmoja wao (wasanii na wenye uwezo wa kuwaongoza) kwa upande wake aone
anaweza vipi kusimama na kuongeza thamani kwa mwenzake na kupeleka hili
gurudumu mbele.
Ifike muda sasa wasanii waache kulalamika kuwa kuna wanaowabania, au
muziki hauchezwi au serikali haisaidii kutatua matatizo yao na kuanza
kuchukua hatua wenyewe kwasababu kwanza ni maisha yao na pili ni faida
kwao, kwani ni wao wenyewe ndio walisababisha kusikilizwa, michango ya
wengine ilikuwepo
ila ni wao walijianza ndipo wengine wakatokea.
Kuna vitu ambavyo serikali haviwezi kutusaidia mpaka tupige hatua
wenyewe, cha kwanza ni hii tasnia, na ili hii tasnia ipige hatua kwa
kasi inayostahili, wasanii na wadau waamue kusimama pamoja na kuanza
kufanya mambo kitaalamu, kila mmoja awajibike kwa upande wake.
Wenye uwezo wa kuwaongoza wasanii wajitokeze, wasanii waamue kutafuta
wenye uwezo wa kuwasimamia. Kila upande ufanye kazi kwa lengo la
kuimarisha tasnia hii. Kuna vitu wasanii wetu wanakosa ambavyo
vinahitaji maamuzi mazuri ili kusonga mbele.
Kwa pamoja tutafika pale tunapotakiwa kuwepo, kwa pamoja tujenge nyumba
moja ambayo kila mtu anahisi anaweza kuijenga bila mchango wa mwingine.
Hii tasnia tamu, hata kwa asiyependa.
Yapasa kushika hatamu, ila mazuri kutenda.
Tena akili timamu, ni nyumba moja twajenga.
Wa karibu yumtamu, na wa mbali hato song
Wednesday, August 31, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment