Thursday, August 4, 2016

Na Dac Popos.
Michuano ya Kimataifa ya Kirafiki (ICC) imeendelea kutimua vumbi kwenye viwanja tofauti, Mabingwa wa ligi kuu ya Uingereza Leicester City walikiona cha mtema kuni baada ya kuchabangwa mabao 4-2 na mabingwa wa Hispania, Barcelona. Iliwachukuwa dakika 25 kwa washindi kuweza kuandika bao la kwanza kupitia kwa kinda wake Munir akiunganisha pasi maridhawa kutoka kwa Messi.

Dakika 8 baadaye yaani dakika ya 33 Suarez akaipatia Barcelona bao la pili kutokana na mpira aliopelekewa na Messi, twaweza sema Lionel Messi ingawa hakufunga bao lolote lakini alikuwa chachu ya ushindi kwa timu yake kwa jinsi alivyokuwa akiiunganisha timu na kutoa pasi nyingi za mwisho zilizozaa mabao na nyingine washambulizi wenzake walishindwa kuzitumia vema.
Kunako dakika ya 45 Munir kwa mara nyingine tena alirejea kambani akiifungia Barcelona bao la tatu, na kufanya matokeo kuwa 3-0 hadi kumalizika kwa kipindi cha kwanza.Kipindi cha pili Leicester City waliingia kitofauti kabisa hasa baada ya kuingia kwa mchezaji Mussa waliyemsajili toka timu ya CSK Moscow kwani dakika moja ya kipindi cha pili mchezaji huyo akaipatia timu yake bao la kwanza kwa kuwafungisha tela wchezaji watatu wa Barcelona toka katikati ya uwanja.

Dakika ya 65 Mussa akaipatia Leicester City bao la pili kwa shuti kali ndani ya boksi alipopata pasi toka kwa Marka aliye mnyang'anya mpira mlinzi J.Alba, na kufanya matokeo kuwa 3-2, lakini kuna msemo usemao anaye jua anajua tu, kwani dakika ya dakika ya 83 kinda mwingine wa Barcelona Mujica aliipatia timu yake bao la nne baada ya walinzi wa Leicester kuzembea kuuondo mpira kwenye eneo la hatari na kumpa mwanya mfungaji kuutumbukiza mpira wavuni. Hadi mwisho wa mchezo huo uliopigwa huko Stockholm Sweden,Barcelona 4 na Leicester City 2.
Nako katika uwanja wa US Bank jimboni Minneapolis nchini Marekani, timu ya Chelsea iliizamisha AC Milan kwa mabao 3-1 katika mchezo wa kusisimua. Dakika ya 24 alikuwa ni mchezaji Traole aliyeanza kufungua kitabu cha mabao kwa kufunga bao la kwanza kwa kichwa kufuatia kuuwahi mpira uliotemwa na kipa wa Milani kutokana na shuti kali la V.Mosess.
Milan walisawazisha bao hilo dakika ya 38 kwa mpira wa adhabu ndogo iliyopigwa kifundi na Bonaventura na kwenda moja kwa moja wavuni.Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa timu hizo kuwa sare ya bao 1-1.Kipindi cha pili mnamo dakika ya 69 Chelsea walipata penati baada ya mlinzi mmoja wa Milan kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari na mwamuzi akaamuru ipigwe penati,ambapo Oscar hakufanya ajizi akaiweka kambani.
Oscar alirudi tena kimiani kuiandikia timu yake ya Chelsea bao la tatu kwenye dakika ya 86 akiitumia pasi nzuri ya Willian.Hivyo hadi kipyenga cha kumaliza mchezo kinapulizwa Chelsea waliibuka kidedea dhidi ya Milan kwa mabao 3-2.
Naye kocha Carlo Ancelotti wa Bayern Munich amedai timu yake itakuwa ya kutisha sana na vijana wake walicheza vizuri sana licha ya kupata kichapo cha bao 1-0 toka kwa Real Madrid. Timu hizi ziliumana vilivyo katika uwanja wa Met Life huko Rutherford, New Jersey nchini Marekani.

Mchezo ulikuwa wa kasi sana na wachezaji wengi vijana kuonyesha viwango vya juu mno. Kosa kosa za hapa na pale zilitawala mchezo, Mchezaji Alaba wa Bayern alijiona si mwenye bahati baada ya mashuti yake mawili kugonga mtambaa panya na kutoka nje.Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa timu kutofungana yaani 0-0.

Kipindi cha pili hakikuwa na mabadiliko ya kimfumo hata baada ya kila timu kufanya mabadiliko ya wachezaji,hadi ilipofika dakika ya 78 pale mchezaji wa Madrid Dannilo alipoipati timu yake bao pekee katika mchezo huo.Kuingia kwa bao hilo kuliufanya mchezo kuchangamka zaidi na timu zote kushambuliana kwa zamu lakini matokeo hayakubadilika.
Huko nchini Uingereza timu ya Manchester United ilitoshana nguvu na timu ya Everton kwa kutokufungana (0-0), kwenye mchezo wa hiari ulioandaliwa na mchezaji Wayne Rooney wa Man U (W,Rooney Charity Match).

Katika mtanange huo wa heshima kwa Rooney kuitumikia Manchester United kwa zaidi ya miaka 10, mapato ya mchezo huo yamepelekwa kwenye vituo vinne vy watoto ambavyo yeye amevichagua.Ndani ya dimba la Old Trafford Wayne Rooney alipata taabu kwani mara kwa mara alikuwa akizomewa na mashabiki wa Everton, timu ambayo aliwahi kuichezea kabla ya kujiunga na Man U.

Ibrahimovich aliikosesha ushindi timu yake mara kadhaa hasa kwa nafasi alizo kuwa anabaki yeye na kipa wa Everton (one against one) na mara zote hizo kipa huyo amekuwa imara kuokoa michomo hiyo.Pia Romeo Lukaku kwa upande wa Everton alikuwa mwiba mkali kwa walinzi wa Man U kwani aliwasumbua vilivyo na kukosa bahati ya kufunga. Hadi mwisho matokeo yalikuwa ni 0-0.

0 comments:

Post a Comment