Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amewaagiza viongozi wote wa kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Kitongoji hapa
nchini kufuatilia matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili
ya kutoa elimu bila malipo kwa lengo la kudhibiti mianya ya matumizi
mabaya ya fedha hizo.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 01 Agosti, 2016 katika
mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mnadani na kuwajumuisha
wananchi wa Katoro na Buseresere Mkoani Geita.
Katika agizo hilo Dkt. Magufuli amewaonya walimu ambao wameanza kufanya
udanganyifu kwa kuandikisha idadi kubwa ya wanafunzi kuliko idadi halisi
kwa lengo la kupata mgao mkubwa wa fedha za ruzuku na amesema Serikali
itachukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayebainika kufanya hivyo.
"Ninafahamu mgao wa fedha hizo hutolewa kulingana na idadi ya wanafunzi
waliopo, wapo baadhi ya walimu ambao wameanza kuandika wanafunzi hewa
katika shule zao, ili kusudi aletewe hela nyingi kuliko idadi ya
wanafunzi waliopo, wanafunzi kama wapo laki nne yeye anasema shule yangu
hii ina wanafunzi laki tano, ili kusudi hela zikija za wanafunzi laki
tano, za wanafunzi laki moja wagawane.
"Napenda nitoe wito kwa walimu Tanzania nzima, mnatafuta matatizo,
narudia mnatafuta matatizo, msijaribu kula hela ya Serikali" Amesema
Rais Magufuli.
Pamoja na agizo hilo, Rais Magufuli pia ametaka viongozi wa ngazi zote
katika Mikoa kuhakikisha wana takwimu za idadi ya wanafunzi katika shule
zote zilizopo katika maeneo yao ili kurahisisha ufuatiliaji wa fedha
hizo na amesema kuwa kuanzia sasa ataanza kutembelea shule kwa
kushitukiza na kwamba kiongozi atakayeonekana kutojua takwimu itakuwa ni
uthibitisho kuwa hatoshi kuendelea na wadhifa alionao.
"Na nitoe wito kwa viongozi wa Mikoa, Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya,
Wakurugenzi, Makatibu Tarafa, Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji,
kila mmoja awe na idadi ya wanafunzi waliopo katika shule zao, hatutaki
kuwapunja wanafunzi hela ambayo wanatakiwa kupata, lakini pia hatutaki
kutoa hela ambayo haitakiwi" Amesisitiza Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ametumia mkutano huo kueleza juhudi mbalimbali
zilizofanywa na Serikali yake ya Awamu ya Tano, kutekeleza ahadi yake
ya kujenga Tanzania Mpya pia amewataka viongozi na watendaji wa Serikali
kutekeleza wajibu wao kwa kutembelea wananchi wanaowaongoza badala ya
kukaa muda mwingi ofisini huku akisisitiza ofisi hizo kuwepo katika
maeneo yenye shughuli husika.
Aidha, Dkt. Magufuli amekosoa utaratibu unaotumiwa na Halmashauri nyingi
za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya kutumia mawakala katika ukusanyaji
wa mapato ya Halmashauri akisema mawakala hao wamekuwa wakitumia
utaratibu huo kukusanya fedha nyingi na kisha kuwasilisha kiasi kidogo
katika Halmashauri husika.
"Hivi kwa nini Halmashauri msingekuwa na maafisa wenu wazuri na mkawa na
mashine za kielektroni kwa ajili ya kukusanya fedha? Amehoji Dkt.
Magufuli na kuongeza kuwa;
"Tena mawakala wengine ndio hao hao wamekuwa wakikusanya kodi hata kwa
wananchi wanyonge wenye vibiashara vidogo vya kuuza mchicha bila hata
kuwaonea huruma"
Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amemaliza
ziara yake ya siku nne katika Mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga na
Geita na yupo nyumbani kwake Chato Mkoani Geita kwa mapumziko mafupi.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Chato
Home
»
Udaku
» Taarifa Toka Ikulu: Rais Magufuli Katoa Maagizo Mazito Kwa Viongozi Wote Hapa Nchini, Pia Katoa Onyo Kali Kwa Walimu
Tuesday, August 2, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment