Imefichuka! Kifo cha Askofu wa Kanisa la Taliteha, Ubungo jijini Dar,
Fred Mwarusi (45) kilichotokea chumbani kwake, Makuburi, Jumapili
iliyopita kimezua mengi na mazito, Amani limefuatilia kwa kina.
Mwili wa marehemu huyo ulibainika na majirani baada ya kusikia harufu
kali kutokea kwenye chumba chake kutokana na kutomwona akiingia wala
kutoka kwa siku kadhaa.
Kwa mujibu wa chanzo makini, kabla ya kifo chake, Askofu Mwalusi
alijifungia chumbani mwake kwa siku kadhaa nyuma kwa ajili ya kufanya
maombi ya uponyaji kwa maradhi yaliyokuwa yakimsumbua ambayo
hayajajulikana mara moja.
ALIKATAA KWENDA HOSPITALI
“Askofu Mwalusi alikuwa akisumbuliwa na maradhi f’lani hivi, yalimfanya
afya yake kudhoofu. Majirani zake na waumini wake walimshauri mara kwa
mara kwenda kutibiwa hospitali ili arejeshe afya yake, lakini alikuwa
akigoma kwa maelezo kwamba, atafanya maombi, atapona kwa Jina la Yesu.
“Alikuwa akisema dawa pekee kwenye matatizo yake ya kiafya ni maombi tu
na kuonesha kuwashangaa sana waliokuwa wakimshauri habari ya kwenda
hospitali,” kilisema chanzo.
MMOJA WA MAJIRANI ANENA
Akizungumza na Amani juzi kwenye msiba wa askofu huyo, mmoja wa majirani
zake aliyekataa katakata jina lake kuandikwa gazetini, alisema siku ya
mwisho kumuona marehemu huyo ilikuwa Ijumaa ya Julai 29, mwaka huu
ambapo aliingia ndani kwake halafu akasikika akifanya maombi kwa
kumuomba Mungu ampe afya njema.
“Nilimsikia akimwomba Mungu ampe afya njema. Lakini baada ya maombi
hayo ya nguvu, nikamsikia akikemea pepo kwa sauti ya chini sana kisha
sikumsikia tena mpaka leo (Jumapili) ndiyo tukaanza kusikia harufu
ikitoka chumbani.”
WASIWASI ULIANZA
“Lakini kuna wakati tuliingiwa na wasiwasi kwa kutomuona mwenzetu
akifungua mlango wake tangu Ijumaa jambo ambalo halikuwa la kawaida
kwake. Alikuwa mtumishi wa Mungu mwenye harakati za kiroho kila wakati,
akiingia na kutoka, pengine akiwa anaimba nyimbo mbalimbali.”
“Kufuatia hali hiyo, tuliambizana kuwa tupige simu polisi ambao
walifika hapa na kuvunja chumba chake, wakamkuta amefariki dunia,”
alisema jirani huyo.
SERIKALI YA MTAA
Akizungumzia tukio hilo Jumatatu iliyopita, Mwenyekiti wa Serikali ya
Mtaa wa Makuburi Kibangu, Moshi Kaftani alisema alipewa taarifa za kifo
cha mtumishi huyo wa Mungu na mmiliki wa nyumba, Peter Mrema ambapo
alishirikiana na polisi kuvunja mlango na kumkuta ameshafariki dunia
huku kukiwa na harufu kali chumbani humo.
“Huyu marehemu ni mwananchi wangu ambaye alikuwa askofu na baadhi ya
waumini wake ni wale pale unaowaona na wachungaji wake walikuwepo hapa
lakini sasa hivi wameshaondoka.”
ALIKATAA KUOA MPAKA…
“Marehemu licha ya kuwa na umri wa miaka 45 lakini hakuwa na mke wala
mtoto. Alipokuwa akiulizwa sababu ya kuishi bila mke alisema anasubiri
aoteshwe na Mungu kwa kuoneshwa ndotoni ndiyo amuoe.
“Licha ya kuisubiri ndoto hiyo kwa muda mrefu lakini haikuwa imemtokea mpaka umauti ulipomfika,” alisema mwenyekiti huyo.
POLISI WATOA MWILI, MAJIRANI WALIA
Paparazi wetu aliushuhudia mwili wa baba askofu ukitolewa nyumbani hapo
alipokuwa akiishi na Askari wa Kituo cha Polisi Mbezi Louis jijini Dar
kwa ajili ya kwenda kuufanyia uchunguzi huku majirani zake wakisikitika,
wengine wakilia kwa uchungu.
MZOZO WA MAZISHI?
Juzi Jumanne, kulidaiwa kuibuka kwa mzozo wa eneo sahihi la kumzikia
marehemu huyo ambapo, baadhi ya ndugu walisema asafirishwe kwenda Mbeya
lakini mama wa marehemu akisema azikwe jijini Dar. Hata hivyo,
mwenyekiti wa serikali ya mtaa alikanusha kuwepo kwa mzozo.
Mwili wa marehemu ulizikwa Jumanne iliyopita kwenye Makaburi ya Ubungo
Maji jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na waumini wake, majirani na
wachungaji huku ibada ya mazishi ikiongozwa na Askofu David Mwasota wa
Kanisa la Naioth Gospel Assembly la jijini Dar.
KAMANDA WA POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime alithibitisha kutokea kwa tukio hilo bila kufafanua zaidi.
Waandishi: Richard Bukos na Gladness Mallya.
Friday, August 5, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.